KUSOMA KITABU CHA ZABURI      DAY 08

| Makala

 

Zaburi 36

1  Kuasi kwake yule mwovu hunena moyoni mwake, Hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yake.

2  Kwa maana hujipendekeza machoni pake Kuwa upotovu wake hautaonekana na kuchukiwa.

3  Maneno ya kinywa chake ni uovu na hila, Ameacha kuwa na akili na kutenda mema.

4  Huwaza maovu kitandani pake, Hujiweka katika njia mbaya; ubaya hauchukii.

5  Ee Bwana, fadhili zako zafika hata mbinguni, Uaminifu wako hata mawinguni.

6  Haki yako ni kama milima ya Mungu, Hukumu zako ni vilindi vikuu, Ee Bwana, unawaokoa wanadamu na wanyama.

7  Ee Mungu, jinsi zilivyo na thamani fadhili zako! Wanadamu huukimbilia uvuli wa mbawa zako.

8  Watashibishwa kwa unono wa nyumba yako, Nawe utawanywesha mto wa furaha zako.

9  Maana kwako Wewe iko chemchemi ya uzima, Katika nuru yako tutaona nuru.

10  Uwadumishie wakujuao fadhili zako, Na wanyofu wa moyo uaminifu wako.

11  Mguu wa kiburi usinikaribie, Wala mkono wa wasio haki usinifukuze.

12  Huko ndiko walikoanguka wafanyao maovu; Wameangushwa chini wasiweze kusimama.


 


 

Zaburi 37

1  Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya, Usiwahusudu wafanyao ubatili.

2  Maana kama majani watakatika mara, Kama miche mibichi watanyauka.

3  Umtumaini Bwana ukatende mema, Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.

4  Nawe utajifurahisha kwa Bwana, Naye atakupa haja za moyo wako.

5  Umkabidhi Bwana njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya.

6  Ataitokeza haki yako kama nuru, Na hukumu yako kama adhuhuri.

7  Ukae kimya mbele za Bwana, Nawe umngojee kwa saburi; Usimkasirikie yeye afanikiwaye katika njia yake, Wala mtu afanyaye hila.

8  Ukomeshe hasira, uache ghadhabu, Usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya.

9  Maana watenda mabaya wataharibiwa, Bali wamngojao Bwana ndio watakaoirithi nchi.

10  Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, Utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo.

11  Bali wenye upole watairithi nchi, Watajifurahisha kwa wingi wa amani.

12  Asiye haki hunuia mabaya juu ya mwenye haki, Na kumsagia meno yake.

13  Bwana atamcheka, Maana ameona kwamba siku yake inakuja.

14  Wasio haki wamefuta upanga na kupinda uta, Wamwangushe chini maskini na mhitaji, Na kuwaua wenye mwenendo wa unyofu.

15  Upanga wao utaingia mioyoni mwao wenyewe, Na nyuta zao zitavunjika.

16  Kidogo alicho nacho mwenye haki ni bora Kuliko wingi wa mali wa wasio haki wengi.

17  Maana mikono ya wasio haki itavunjika, Bali Bwana huwategemeza wenye haki.

18  Bwana anazijua siku za wakamilifu, Na urithi wao utakuwa wa milele.

19  Hawataaibika wakati wa ubaya, Na siku za njaa watashiba.

20  Bali wasio haki watapotea, Nao wamchukiao Bwana watatoweka, Kama uzuri wa mashamba, Kama moshi watatoweka.

21  Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu.

22  Maana waliobarikiwa na yeye watairithi nchi, Nao waliolaaniwa na yeye wataharibiwa.

23  Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana, Naye aipenda njia yake.

24  Ajapojikwaa hataanguka chini, Bwana humshika mkono na kumtegemeza.

25  Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula.

26  Mchana kutwa hufadhili na kukopesha, Na mzao wake hubarikiwa.

27  Jiepue na uovu, utende mema, Na kukaa hata milele.

28  Kwa kuwa Bwana hupenda haki, Wala hawaachi watauwa wake. Wao hulindwa milele, Bali mzao wa wasio haki ataharibiwa.

29  Wenye haki watairithi nchi, Nao watakaa humo milele.

30  Kinywa chake mwenye haki hunena hekima, Na ulimi wake husema hukumu.

31  Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake. Hatua zake hazitelezi.

32  Mtu asiye haki humvizia mwenye haki, Na kutafuta jinsi ya kumfisha.

33  Bwana hatamwacha mkononi mwake, Wala hatamlaumu atakapohukumiwa.

34  Wewe umngoje Bwana, Uishike njia yake, Naye atakutukuza uirithi nchi, Wasio haki watakapoharibiwa utawaona.

35  Nimemwona mtu asiye haki mkali sana, Akijieneza kama mwerezi wa Lebanoni.

36  Nikapita na kumbe! Hayuko, Nikamtafuta wala hakuonekana.

37  Umwangalie sana mtu mkamilifu, Umtazame mtu mnyofu, Maana mwisho wake mtu huyo ni amani.

38  Wakosaji wataangamizwa pamoja, Wasio haki mwisho wao wataharibiwa.

39  Na wokovu wa wenye haki una Bwana; Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.

40  Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa; Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa; Kwa kuwa wamemtumaini Yeye.


 


 

Zaburi 38

1  Ee Bwana, usinilaumu katika ghadhabu yako, Wala usiniadhibu kwa ukali wa hasira yako.

2  Kwa maana mishale yako imenichoma, Na mkono wako umenipata.

3  Hamna uzima katika mwili wangu Kwa sababu ya ghadhabu yako. Wala hamna amani mifupani mwangu Kwa sababu ya hatia zangu.

4  Maana dhambi zangu zimenifunikiza kichwa, Kama mzigo mzito zimenilemea mno.

5  Jeraha zangu zinanuka, zimeoza, Kwa sababu ya upumbavu wangu.

6  Nimepindika na kuinama sana, Mchana kutwa nimekwenda nikihuzunika.

7  Maana viuno vyangu vimejaa homa, Wala hamna uzima katika mwili wangu.

8  Nimedhoofika na kuchubuka sana, Nimeugua kwa fadhaa ya moyo wangu.

9  Bwana, haja zangu zote ziko mbele zako, Kuugua kwangu hakukusitirika kwako.

10  Moyo wangu unapwita-pwita, Nguvu zangu zimeniacha; Nuru ya macho yangu nayo imeniondoka.

11  Wanipendao na rafiki zangu wanasimama mbali na pigo langu; Naam, karibu zangu wamesimama mbali.

12  Nao wanaoutafuta uhai wangu hutega mitego; Nao wanaotaka kunidhuru hunena mabaya; Na kufikiri hila mchana kutwa.

13  Lakini kama kiziwi sisikii, Nami ni kama bubu asiyefumbua kinywa chake.

14  Naam, nimekuwa kama mtu asiyesikia, Ambaye hamna hoja kinywani mwake.

15  Kwa kuwa nakungoja Wewe, Bwana, Wewe utajibu, Ee Bwana, Mungu wangu.

16  Maana nalisema, Wasije wakanifurahia; Mguu wangu ukiteleza wajitukuza juu yangu.

17  Kwa maana mimi ni karibu na kusita, Na maumivu yangu yako mbele yangu daima.

18  Kwa maana nitaungama uovu wangu, Na kusikitika kwa dhambi zangu.

19  Lakini adui zangu ni wazima wenye nguvu, Nao wanaonichukia bure wamekuwa wengi.

20  Naam, wakilipa mabaya kwa mema, Huwa adui zangu kwa kuwa nalifuata lililo jema.

21  Wewe, Bwana, usiniache, Mungu wangu, usijitenge nami.

22  Ufanye haraka kunisaidia, Ee Bwana, wokovu wangu.


 


 

Zaburi 39

1  Nalisema, Nitazitunza njia zangu Nisije nikakosa kwa ulimi wangu; Nitajitia lijamu kinywani, Maadamu mtu mbaya yupo mbele yangu.

2  Nalikuwa sisemi, nalinyamaa kimya, Sina faraja, maumivu yangu yakazidi.

3  Moyo wangu ukawa moto ndani yangu, Na katika kuwaza kwangu moto ukawaka; Nalisema kwa ulimi wangu,

4  Bwana, unijulishe mwisho wangu, Na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani; Nijue jinsi nilivyo dhaifu.

5  Tazama, umefanya siku zangu kuwa mashubiri; Maisha yangu ni kama si kitu mbele zako. Kila mwanadamu, ingawa amesitawi, ni ubatili.

6  Binadamu huenda tu huko na huko kama kivuli; Hufanya ghasia tu kwa ajili ya ubatili; Huweka akiba wala hajui ni nani atakayeichukua.

7  Na sasa ninangoja nini, Ee Bwana? Matumaini yangu ni kwako.

8  Uniokoe na maasi yangu yote, Usinifanye laumu ya mpumbavu.

9  Nimenyamaza, sitafumbua kinywa changu, Maana Wewe ndiwe uliyeyafanya.

10  Uniondolee pigo lako; Kwa uadui wa mkono wako nimeangamia.

11  Ukimrudi mtu kwa kumkemea kwa uovu wake, Watowesha uzuri wake kama nondo. Kila mwanadamu ni ubatili.

12  Ee Bwana, usikie maombi yangu, Utege sikio lako niliapo, Usiyanyamalie machozi yangu. Kwa maana mimi ni mgeni wako, Msafiri kama baba zangu wote.

13  Uniachilie nikunjuke uso, Kabla sijaondoka nisiwepo tena.


 


 

Zaburi 40

1  Nalimngoja Bwana kwa saburi, Akaniinamia akakisikia kilio changu.

2  Akanipandisha toka shimo la uharibifu, Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua zangu.

3  Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, Nao watamtumaini Bwana

4  Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake, Wala hakuwaelekea wenye kiburi, Wala hao wanaogeukia uongo.

5  Ee Bwana, Mungu wangu, umefanya kwa wingi Miujiza yako na mawazo yako kwetu; Hakuna awezaye kufananishwa nawe; Kama ningependa kuyatangaza na kuyahubiri, Ni mengi sana hayahesabiki.

6  Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, Masikio yangu umeyazibua, Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.

7  Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (Katika gombo la chuo nimeandikiwa,)

8  Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.

9  Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa. Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua.

10  Sikusitiri haki yako moyoni mwangu; Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako. Sikuficha fadhili zako wala kweli yako Katika kusanyiko kubwa.

11  Nawe, Bwana, usinizuilie rehema zako, Fadhili zako na kweli yako na zinihifadhi daima.

12  Kwa maana mabaya yasiyohesabika Yamenizunguka mimi. Maovu yangu yamenipata, Wala siwezi kuona. Yamezidi kuliko nywele za kichwa changu, Na moyo wangu umeniacha.

13  Ee Bwana, uwe radhi kuniokoa, Ee Bwana, unisaidie hima.

14  Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu.

15  Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe!

16  Washangilie, wakufurahie, Wote wakutafutao. Waupendao wokovu wako Waseme daima, Atukuzwe Bwana.

17  Nami ni maskini na mhitaji, Bwana atanitunza. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, Ee Mungu wangu, usikawie.


 


 


 SADAKA